Jinsi ya kucheza bahati nasibu ya viza ya kuishi Marekani kwa mwaka 2015
KILA mwaka Marekani inatoa nafasi kwa watu 55,000 kupata bahati ya kuwa na viza (kibali cha uhamiaji) kitakachowawezesha kuishi, kusoma na kufanya kazi Marekani. Viza hii ni tofauti na viza nyingine zozote zinazotolewa na Wamarekani na inawezekana labda ni aina ya viza inayotolewa mahali pekee duniani – kwa njia ya bahati nasibu.
Si nchi zote duniani zinaweza kutoa washindi isipokuwa nchi ambazo zimetajwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani (State Department). Kwa mfano mwaka huu Nigeria haiwezi kutoa washindi wa viza hiyo kwa sababu imetajwa kama nchi ambayo haina nafasi ya kufanya hivyo.
Nchi nyingi zilizoendelea kama Japan, Ujerumani n.k nazo hazimo humo. Kwa Afrika nchi nyingi zinahusika isipokuwa Nigeria. Tanzania ni nchi mojawapo ambayo mwaka huu kama miaka mingi iliyopita imetajwa kama wananchi wake wanaweza kucheza bahati nasibu hiyo.
Bahati nasibu hii inaanza katika kipindi cha mwezi mmoja tu na matokeo yanatoka katikati ya mwaka unaofuatia na washindi wanatakiwa wakamilishe taratibu zote za kuhamia mwaka unaofuatia.
Kwa ujumla inachukua kama miaka miwili hivi kwa mtu kuweza kukamilisha taratibu za kwenda Marekani endapo ataenda huko.
Jambo la msingi kukumbuka ni kuwa hii ni bahati nasibu; kwa maana ya kwamba mamilioni ya watu wataingiza majina na taarifa zao na siku ya uchaguzi kompyuta itachagua washindi kwa nasibu. Kwa vile ni bahati nasibu hakuna mtu anayeweza kukuhakikishia kuwa utashinda!
Wapo waliocheza mara nyingi na zote wameshinda na wengine ambao waliwachezea rafiki zao au ndugu zao wakajikuta wenzao wameshinda na wao wenyewe wameshindwa; ndiyo maana ya nasibu.
Kwa muda mrefu nchi nyingi za Kiafrika hasa za Magharibi zimekuwa zikifuatilia hili na wananchi wao wengi wameweza kuhamia Marekani na kupata nafasi mbalimbali za kazi, masomo na maisha. Nchi kama Ghana, Kenya, Liberia na Cameron zimetoa watu wengi tu huko.
Bahati mbaya Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zina ushiriki mdogo ama kwa sababu watu wengi hawajui, au kutokana na mchakato mzima kutokueleweka na wengine wakitapeliwa na makampuni au watu ambao wanawaahidi kuwa wanaweza kusaidia kushinda. Narudia, hakuna mtu au taasisi inayoweza kukupa nafasi ya kushinda bahati nasibu hii.
Ni ukweli huu umenisukuma dakika hizi za majeruhi – zimebakia chini ya wiki mbili kabla ya muda wa kucheza bahati nasibu kufungwa – unafungwa Novemba 2, 2013 kuwapa nafasi watu wengi kujua na kutumia nafasi hii kama watakidhi vigezo na kujaza taarifa zao kwa usahihi.
Kubwa la kukumbuka ni kuwa ili kuweza kutuma taarifa zako ili uingie kwenye shindano hili ni muhimu kuwa na uhakika wa kompyuta au mtandao wa intaneti kwani fomu zote za shindano zinatumwa kwa mfumo huu.
Nieleze pia kuwa ni muhimu kufikiria sana kama unataka kucheza bahati nasibu hii hasa kama hauna familia au ndugu Marekani. Marekani ni pagumu sana kama hujui Kiingereza na huna jamaa huku, hivyo kucheza bahati nasibu bila kuwa na ‘mahali pa kufikia’ kunaweza kuwanyima wengine nafasi ya kwenda huko hasa kama unashinda halafu unaamua kutokwenda!
Kabla ya kucheza ni vizuri ujiulize kama kweli unataka kwenda au unabahatisha kuona kama utashinda halafu utajua mbele ya safari.
Bahati nasibu hii maarufu kama ‘Green Card Lottery’ au kwa jina rasmi DV-2015 Lottery (Diversity Visa) inamuwezesha mtu aliyeshinda kupata mojawapo kati ya viza 55,000 ambazo Marekani inatoa kila mwaka kwa nchi ambazo zinaruhusiwa kushiriki.
Viza hizi mtu akishinda anapata nafasi ya kuishi Marekani na hata baadaye kuweza kupata uraia wa Marekani akitimiza masharti. Kila mwaka maelfu ya watu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanapata nafasi hizo na wanazitumia vizuri kuja kuanza maisha Marekani.
Hata hivyo, Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo waombaji wake ni wachache kila mwaka kulinganisha na nchi kama Kenya, Ghana n.k. La muhimu ni kufuata masharti yake muhimu ambayo si magumu sana.
- Muda wa mchezo wa bahati nasibu: Muda ilikuwa tangu Oktoba 1 hadi Novemba 2, 2013.
- Ni muhimu kujibu maswali yote yanayotaka taarifa muhimu.
- Ni muhimu kuzingatia matakwa ya picha za ‘passport’. Watu wengi wanajikuta wanakataliwa kwa sababu hawakutimiza masharti ya picha. Angalia chini.
- Ni fomu moja tu inaruhusiwa kuingizwa kwa mtu yule yule; ukiingiza zaidi ya fomu moja unakataliwa moja kwa moja.
- Hakuna gharama ya kujaza fomu hii kwenye tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje Marekani.
- Si lazima kuajiri mtu kukufanyia kwani yeyote anayejaza kwa niaba yako naye itampasa aende kwenye website hiyo hiyo.
- Ukishatuma fomu yako utapata ukurasa wa uthibitisho ambao utakuwa na taarifa za jinsi ya kufuatilia matokeo. Hakikisha unachapisha ukurasa huu na kutunza taarifa zake kwani pasipo kuwa nazo hautaweza kujua matokeo yakoje.
- Kuna mambo 14 ambayo utatakiwa kuyapatia taarifa au kujaza kwenye fomu hiyo. Ni vizuri kama utayaandika mambo haya pembeni kwanza ili usihangaike kutafuta wakati unajaza fomu hiyo.
- JINA: Jina lako la familia, jina la kati na jina la mwanzo kama yanavyoonekana kwenye passport au kitambulisho chako.
- TAREHE YA KUZALIWA: Tarehe, mwezi, mwaka.
- JINSIA: Ni mwanamke au mwanamume
- MJI ULIOZALIWA: Kama inavyoonekana kwenye cheti chako cha kuzaliwa au passport yako.
- NCHI ULIYOZALIWA: Kama inavyoonekana kwenye pasi ya kusafiria
- NCHI INAYORUHUSIWA KUCHEZA LOTTO HII: Kwa kawaida ni nchi ile ile uliyozaliwa. Hii si lazima iwe nchi ambayo unaishi wakati huu. Kwa mfano, Mtanzania anayeishi Ujerumani ataweka nchi yake kama Tanzania.
- INGIZA PICHA: Unatakiwa kuingiza picha zote za hivi karibuni za kwako, mwenza wako na watoto wote ambao utakuwa umewaingiza kwenye fomu hii. Picha hizi ni LAZIMA ziwe zilizopigwa kwa kamera za kidijitali (digital camera).
- Picha ni za mtu mmoja mmoja si za kundi. Picha hizi zisiwe zimechezewa kwa namna yoyote; ni lazima ziwe za rangi halisi hivyo usijaribu kuzibadilisha kwa namna yoyote. Ukitumia ‘scanner’ kuchukua picha ni lazima uweke maelekezo kuwa iwe ni kwa ‘true colors’.
- Anayepigwa picha ni lazima awe amesimama anaangalia mbele bila kupindisha kichwa kwa namna yoyote ile (asiangalie chini, juu au pembeni). Wanataka kuona uso mzima.
- Picha ipigwe ambapo nyuma hakuna rangi yoyote isipokuwa nyeupe au rangi angavu. Usivae miwani ya jua au kofia au kitu chochote ambacho kitaficha sura. Picha zinatakiwa zihifadhiwe katika mfumo wa JPG, si mfumo mwingine wowote.
- ANUANI YA BARUA: Hapa weka anuani yako ambayo barua zinaweza kukufikia kwa njia ya posta. Usisahau kuweka mji na nchi na kama iko kwa niaba ya mtu mwingine basi usisahau kuweka C/O (Care Of).
- NCHI UNAYOISHI SASA: Unaweza kuwa Mtanzania unayeomba nafasi hiyo ukiwa nchi nyingine unakoishi au kufanya kazi au hata kusoma. Na hapa inaweza pia ndiyo anuani yako ya barua ya hapo juu.
- NAMBA YA SIMU: (Hii si lazima, lakini kama unayo weka).
- ANUANI YA EMAIL: Hii si kwa ajili ya kupata taarifa za ushindi wako. Ni kuwa kama umeshinda na ukajibu kupitia mfumo wao basi watakutumia e-mail kwa maelekezo mengine kuhusiana na ushindi wako.
- KIWANGO CHA JUU CHA ELIMU: Kwa ujumla mtu aliyetumia mafunzo yenye jumla ya miaka 12 kuanzia shule ya msingi na sekondari au elimu ya ufundi. Ushahidi wa elimu hii utatakiwa kuwasilishwa kwa mtu aliyeshinda wakati anaenda kupata viza yake ubalozini. Mtu anaweza pia kucheza bahati nasibu hii kama amekuwa katika ajira isiyopungua miaka miwili katika mitano iliyopita ambayo inahitaji mafunzo yasiyopungua miaka miwili.
- HALI YAKO YA NDOA: Andika kama umeoa, kuolewa, uko peke yako, umeachika au mmetengana. Kama una mwenza wako basi unatakiwa kuweka taarifa zote za jina, mahali pa kuzaliwa, nchi ya kuzaliwa, tarehe ya kuzaliwa, picha yake.
- IDADI YA WATOTO: Orodhesha watoto wako wote walio chini ya umri wa miaka 21 ambao hawajaoa/olewa.
- Weka majina yao kamili, tarehe za kuzaliwa, mahali pa kuzaliwa na nchi ya kuzaliwa. Haijalishi kama watoto hao wanaishi na wewe au kama unataka uende nao Marekani kama ukishinda.
- Ambatanisha picha kwa utaratibu ule ule wa kuweka picha hapo juu.
- Zingatia kuweka watoto wote ambao wako hai, ambao unawalea na wako chini ya uangalizi wako na hata watoto wa mwenza wako ambao hamkuzaa pamoja.
- Wote waliocheza bahati nasibu hii ya DV-2015 watachaguliwa na kompyuta kupata washindi.
- Waliocheza bahati nasibu watatembelea ukurasa wa Entrant Status Check kwenye tovuti ya bahati nasibu kuangalia kama wameshinda.
- Ukurasa huu utaanza kupatikana kuanzia Mei 1, 2014 hadi Juni 30, 2015
- Ukiingia kwenye ukurasa huo na kukuta jina lako limeshindwa utaelekezwa kwenye ukurasa mwingine ambapo utapata taarifa zote muhimu kuhusiana na ada za viza na taratibu nyingine. Njia pekee ya kujua kama umeshinda ni kuingia katika tovuti hiyo. Usitarajie barua au e-mail kupata taarifa za ushindi wako.
- Taratibu zote za kushughulikia viza na kuhamia Marekani zinatakiwa ziwe zimekamilika ifikapo Septemba 30, 2015. Nje ya hapo hata kama umeshinda unapoteza nafasi hiyo. Hii ni kwa mwombaji mkuu pamoja na wategemezi wake (familia).
- Mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 anaweza kucheza. Kumbuka si lazima uwe unajua Kiingereza alimradi uwe na elimu ya kufikia sekondari kama ilivyo hapo juu.
KUMBUKA HAHUHITAJI MSAADA WANGU AU WA MTU YEYOTE, kwani unaweza kwenda mwenyewe na kufuata maelekezo hayo hapo juu kwenye ukurasa wa bahati nasibu hiyo hapa na ukifuata maelekezo hahuhitaji kumlipa mtu yeyote kwani ni bure:http://www.dvlottery.state.gov
No comments:
Post a Comment